Tamko la Msemaji wa Katibu Mkuu – kuhusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
31 Oktoba 2025
Tanzania
Katibu Mkuu ana wasiwasi mkubwa kuhusu hali ilivyo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba, ikiwa ni pamoja na taarifa za vifo na majeruhi wakati wa maandamano. Analaani vifo vilivyotokea na anatuma salamu za rambirambi kwa familia za waathirika.
Anasisitiza umuhimu mkubwa wa kulinda haki za msingi, hususan haki ya kukusanyika kwa amani na uhuru wa kujieleza, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa taarifa. Anatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina na usio na upendeleo kuhusu tuhuma zote za matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Katibu Mkuu pia ana wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa za kutoweka na kukamatwa kwa watu katika kipindi cha kuelekea uchaguzi. Anazihimiza mamlaka kuhakikisha kuwa taratibu za kisheria zinafuatwa kwa wote waliokamatwa, kuhakikisha usalama wao, na kufanya uchunguzi wa kina na wa haki kuhusu tuhuma zote za ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.
Katibu Mkuu anatoa wito kwa wadau wote kuwa na kiasi, kukataa matumizi ya vurugu na kushiriki katika mazungumzo jumuishi na ya kujenga ili kushughulikia malalamiko na kuzuia kuzorota zaidi kwa hali ya usalama. Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia juhudi za kuendeleza mazungumzo, kuimarisha utawala wa kidemokrasia na kukuza amani endelevu nchini Tanzania.
Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu
New York, 31 Oktoba 2025