Winda* alikuwa na umri wa miaka 13 na alikuwa tayari kujiunga na elimu ya sekondari pale baba yake alipomtaka kwenda kufanyiwa ukeketaji. “Aliniambia kuwa sasa nimekua na kwamba ilikuwa ni lazima nifanyiwe ukeketaji ili familia yangu ijivunie nami na kupata heshima katika jamii,” anakumbuka.
Huku madhara ya ukeketaji yakiwa yanajulikana waziwazi – inaweza kuonekana kama vile ni jambo jepesi kusema hapana kwa ukeketaji. Lakini kwa upande wa Winda – na mamilioni ya wanawake na wasichana kote duniani – wanaoishi katika jamii ambako ukeketaji unaonekana kama hatua muhimu katika safari ya kukua na ambako wasichana wasiokeketwa wananyanyapaliwa na mara nyingi hawawezi kuolewa – kukataa kukeketwa maana yke ni kupoteza jamii yako, familia yako na marafiki zako.
Ukeketaji ni kitendo kilichoharamishwa nchini Tanzania tangu mwaka 1998 na serikali imekuwa ikifanya kila juhudi kukomesha vitendo hivyo, kam inavyoelezwa katika ajenda za maendeleo za kitaifa, kikanda na dunia, na kama inavyoshuhudiwa na kupungua kwa vitendo hivyo nchini. Hata hivyo, bado kuna tofauti kutoka mkoa mmoja hadi mwingine ambapo Mkoa wa Mara – alikozaliwa Winda – asilimia 32 ya wanawake wenye miaka 15 hadi 49 bado wanakeketwa.
Winda alipata elimu kuhusu madhara ya ukeketaji baada ya wanaharakati wa kukomesha ukeketaji kutembelea shuleni alikokuwa akisoma. Alijua kwamba endapo angalifanyiwa ukeketaji basi angalipatwa na madhara ya muda mfupi na muda mrefu, au hata kifo, na hayo yalimwogofya sana. Aliwambembeleza wanafamilia yake wasimfanyie ukeketaji – ambapo aliungwa mkono na kaka yake – lakini walikataa katakata kumsikiliza.
Winda alifanya uamuzi wa kishujaa na kutoroka nyumbani kwao ambapo alitembea kwa siku tatu hadi Kituo cha Polisi cha Mugumu. Hapo alikutana na Sijari, askari polisi anayeshughulikia Dawati la Jinsia na Watoto, ambaye alimpeleka Winda katika makazi salama chini ya taasisi ya Hope for Women and Girls, Tanzania, (Matumaini kwa Wanawake na Wasichana) huko Serengeti. Hivi sasa Winda ana umri wa miaka 17 na bado anaishi katika makazi hayo salama. Anapata msaada wa kieleimu na anasema ndoto yake ni kuwa daktari.
Winda ni miongoni mwa wanawake vijana wengi wanaokataa ukeketaji nchini Tanzania, na hayuko peke yake. Vijana, wazazi na jamii wamefanya uamuzi kwamba hawataki kuendelea vitendo hivyo ya ukeketaji, kwamba wanapenda watoto wao wawe na hatma njema maishani – dunia iliyo bora zaidi na yenye usawa kwa binti zao.
UNFPA imedhamiria kuendelea kuongeza juhudi za kufikia lengo la kukomesha ukeketaji ifikapo mwaka 2030 – kuanzia kuimarisha mazingira ya sera nchini Tanzania hadi kuvuka mipaka katika kuimarisha mifumo ya kinga na utoaji mwitikio; kuongeza utoaji elimu katika jamii na shule na kupanua taratibu nyingine za hatua za makuzi ya mtu.
Tunapoelekea katika Siku ya Kimataifa ya Kutovumilia Kabisa – kwa wasichana kama Winda na wengineo wengi kama yeye – tunatoa wito unaorindika kote duniani: “Huu si wakati wa kutochukua hatua: Unganeni, toeni fedha na chukueni hatua kukomesha ukeketaji”.