Kongamano la AfCFTA la Wanawake na Vijana Wafanyabiashara
.
- Mheshimiwa, Bw. Wamkele Mene, Katibu Mkuu wa AfCFTA,
- Viongozi na Maofisa Waandamizi wa Serikali kutoka barani Afrika,
- Washirika wa Maendeleo, Wenzangu kutoka Umoja wa Mataifa, Wanawake na Vijana Wafanyabiashara,
- Wageni Waalikwa, Mabibi na Mbwana
Habari za Mchana
Wanawake Oyee, Vijana Oyee
Tafadhali mniruhusu nianze kwa kutoa pongezi kwa kila mmoja aliyeshiriki kuandaa kongamano hili lililofanikiwa sana, wakiwemo: Sekretarieti ya Mpango wa AfCFTA, Serikali mbalimbali, UN Women, UNDP, na washirika wengine wote ambao walisaidia kongamano hili. Pia ninawatambua washiriki kutoka vyama vya kitaifa vya wasafirishaji bidhaa nje, mabaraza ya biashara, vikundi vya wanawake na vijana na vyama vya kijamii, kwa ushiriki wao motomoto katika majadiliano, matukio na maonyesho yaliyofanyika hapa kwa siku kadhaa.
Tunaishukuru Tanzania kwa uongozi wake katika kuwa wenyeji wa tukio hili, ambalo limewaleta pamoja wadau wa kila aina kutoka katika sekta na nchi tofauti. Kuwaleta pamoja wadau katika jukwaa kama hili ni muhimu katika kuendeleza dira ya pamoja ya aina ya AfCFTA inayozingatia changamoto zinazowakabili wanawake na vijana barani Afrika. Ni muhimu kwamba wanawake, vijana na makundi mengine muhimu wanashiriki pale sera zinapotungwa, ili maoni yao yasaidie kutoa mwanga na kusaidia kuweka sawa masuluhisho yanayopendekezwa dhidi ya changamoto wanazokabiliana nazo katika uendeshaji wa siku hadi siku wa shughuli zao.
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inakadiria kwamba zaidi ya Waafrika milioni 30.4 waliingia kwenye umaskini uliokithiri mwaka 2020 kutokana na madhara ya janga la UVIKO-19, na wengine milioni 38.7 katika mwaka uliofuatia wa 2021. Katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, wanawake ndiyo walioathirika zaidi katika wale waliopoteza kazi, hasa kwa sababu wao ni wengi sana miongoni mwa watumishi wasio kwenye ajira rasmi ambao waliathiriwa vibaya sana na masharti ya kutotoka ndani, kufungwa kwa maeneo ya kazi na pia mipaka ya nchi.
Janga hilo lilikuwa na madhara ya pande tatu kwa vijana wa ukanda huu, yaani: kupoteza kazi na kipato, hatari ya kupungua kwa haki za kazi na kuvurugwa kwa elimu na mafunzo, jambo lililoongeza vikwazo zaidi katika kutafuta kazi, kutafuta upya ajira, au kuingia kwenye kazi nyingine iliyo bora zaidi.
Ningeweza kutoa ushahidi mwingi zaidi … Ninachotaka kueleza ni kwamba janga hilo lilikuwa na madhara makubwa sana kwa wanawake na vijana. Tunaweza pia kutarajia kwamba madhara ya ongezeko zaidi la bei za mafuta, mbolea, ngano, mahindi na madhara mengine yenye uharibifu yaliyosabaishwa na vita vya Ukraine yataendelea kuwa na athari mbaya dhidi ya wanawake na vijana, kama ambavyo madhara kama hayo yatakavyoendelezwa na mabadilio ya tabianchi.
Muktadha kama huo wa ngazi ya dunia unafanya kongamano hili liwe muhimu zaidi. Benki ya Dunia inakadiria kwamba Mpango wa Eneo Huru la Biashara wa Afrika (AfCFTA) utaimarisha kipato cha Afrika kwa Dola za Marekani bilioni 450 ifikapo mwaka 2035 na kuongeza usafirishaji bidhaa miongoni mwa nchi za Kiafrika kwa zaidi ya asilimia 81. Makubaliano haya yanatarajiwa kuwaondoa watu milioni 30 kutoka katika umaskini uliokithiri na wengine milioni 68 kutoka katika umaskini wa kadiri.
Mpango wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) unaleta matumaini kwa bara katika kukabiliana na changamoto za kidunia. ‘Kujenga upya vizuri zaidi’ sasa umekuwa msemo wa kawaida katika kipindi cha baada ya UVIKO-19 na Mpango wa AfCFTA ni nguzo muhimu, kwa bara la Afrika, katika kujenga upya vizuri zaidi. Mpango huu unatoa fursa ya kuongeza kasi ya biashara katika ukanda huu na kuitumia vizuri zaidi kwa ukuaji na maendeleo endelevu na kuhakikisha ustahimilivu na mabadiliko chanya ya kiuchumi.
Kongamano lililofanyika wiki hii, na Azimio lake ni muhimu katika kuhakikisha kwamba manufaa yanayotarajiwa ya kiuchumi ya AfCFTA yanakuwa jumuishi, na kwamba ukosefu wa usawa uliopo hautawazuia wanawake na vijana katika kutumia fursa hizo zinazoletwa na mpango huo. Nina imani kwamba Tamko hilo litasaidia kujenga vema Protokali ya Mpango wa AfCFTA wa Wanawake na Vijana Wafanyabiashara, kusaidia kutatua changamozo zinazowakabili wanawake na vijana nchini Tanzania, Afrika Mashariki na bara zima la Afrika.
Kama Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, sisi tumekuwa tukiwaunga mkono wanawake na vijana nchini kwa miaka mingi, ikiwemo katika elimu, mafunzo ya ufundi na mafunzo ya stadi za biashara, kilimo, mnyororo wa uongezaji thamani, upatikanaji wa masoko na mitaji, na maeneo mengine. Vile vile tunashirikiana na Serikali na wadau wengine kuandaa mapitio ya sera kwa lengo la kuweka kipaumbele katika mahitaji ya wanawake na vijana. Katika ngazi ya kikanda, Umoja wa Mataifa umesaidia utafiti wa kuimarisha Protokali ya Mapango wa AfCFTA kwa Wanawake na Vijana Wafanyabiashara, ili kuhakikisha maendeleo jumuishi ya kijamii na kiuchumi na kwamba hakuna yeyote atakayeachwa nyuma.
Kama ambavyo baadhi yenu mnafahamu, Umoja wa Mataifa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaina kwa pamoja zilizindua Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Ushrikiano katika Maendeleo Endelevu (UNSDCF) wa kutoka 2022-2027 ambao utasimamia kazi za Umoja wa Mataifa nchini Tanzania katika kipindi cha miaka mitano ijayo na msaada wetu katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na vipaumbele vya taifa vya maendeleo.
Mifumo ya UNSDCFs ni mifumo ya aina mpya ya ushirikiano na Umoja wa Mataifa inayosisitiza ushirikiano miongoni na kati ya wadau mbalimbali ili kuendeleza agenda ya maendeleo. Kupitia Mfumo wa UNSDCF, Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana moja kwa moja na wanawake na vijana ili kuwapa stadi na kuwajengea uwezo ili kujenga njia zao endelevu za kujiendeshea maisha.
Vile vile tutashirikiana na washirika kama AfCFTA ili kuwaleta pamoja wadau, kuongeza kasi ya upigaji hatua katika utekelezaji wa SDGs, Agenda ya AU ya 2063 na vipaumbele katika dira ya taifa ya maendeleo.
Kwa mara nyingine ninampongeza kila mmoja kuanzia waandaaji hadi washiriki kwa kufanikisha kwa mafanikio kongamano hili muhimu. Ninatoa wito kwa kila mdau kuchukua hatua ili kufanikisha ufikiwaji wa mpango wa AfCFTA ambayo haiwaachi nyuma wanawake na vijana.
Asanteni sana!