Vituo vya jamii vinavyoungwa mkono na UNHCR vinatoa matumaini kwa wanawake vijana wa Kitanzania
19 Julai 2022
Vijana wa kike wa Kitanzania wakijifunza ufundi mbalimbali kutoka katika vituo vya mafunzo ya ufundi stadi vilivyopo karibu na kambi za wakimbizi.
“Shule ya ufundi ya Malogerwa ilibadilisha maisha yangu. Sasa mimi ni mfanyabiashara, na wakati wangu ujao ni mzuri,” akasema Sporah mwenye umri wa miaka 21.
“Nina kazi sasa na Shirika Lisilo la Kiserikali. Nisingepata nafasi hii bila maarifa niliyopata kutokana na kujifunza ujuzi wa kompyuta,” alisema Yuditha kwa tabasamu pana.
Sporah na Yuditha ni mifano miwili ya mamia ya vijana wa kike wa Kitanzania waliopata ujuzi wa vitendo unaowawezesha kumudu taaluma mbalimbali kutoka katika vituo vya mafunzo ya ufundi stadi vilivyopo pembezoni mwa kambi za wakimbizi katika Wilaya za Kibondo na Kasulu. Mafunzo yanayotolewa na UNHCR na Baraza la Wakimbizi la Denmark ni pamoja na; Jumuiya ya Teknolojia ya Habari (ICT), ushonaji, kutengeneza sabuni, kurekebisha simu, kutengeneza baiskeli, kutengeneza nywele, na kuoka, miongoni mwa mengine.
Sporah ambaye alizaliwa katika familia ya kipato cha chini wilayani Kibondo, alishindwa kuendelea na shule ya msingi kutokana na umaskini. Kadhalika, Yuditha mwenye umri wa miaka 19 kutoka Wilaya ya Kasulu alimaliza elimu yake ya sekondari mwaka 2019 lakini hakuweza kuendelea na elimu ya juu kutokana na matatizo ya kifedha.
Sporah na Yuditha walijiunga na madarasa ya Maloregwa na Nyarugusu, mtawalia, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa viongozi wao wa kijiji. Kufuatia mchakato mkali wa uchunguzi, Sporah alianza madarasa ya ushonaji na kudarizi. "Nilijifunza na kukuza ujuzi katika ushonaji, kudarizi, kubuni, stadi za maisha, na ujuzi wa kifedha ambao umenisaidia kufanya maamuzi sahihi ya kifedha katika biashara yangu," alisema. Baada ya mafunzo hayo, Sporah alipata cherehani ikiwa ni sehemu ya vifaa vya kuanzia, na kwa sasa ameanzisha biashara ambayo inastawi ambapo pia anawafundisha vijana wengine wa kike.
Yuditha, kwa upande mwingine, alifanikiwa kuingia kwenye kozi ya Teknolojia ya Habari (ICT) iliyokuwa na ushindani mkubwa, akiwa mmoja wa wanawake watatu katika darasa la wanafunzi 40. “Nilipokuwa nikikua, sikuzote nilivutiwa nikitazama watu wakichapa na kusogeza kipanya cha kompyuta kwenye maduka ya karibu ya vifaa vya kuandikia. Siku zote nilitamani ningefanya vivyo hivyo siku moja,” anacheka. "Leo hii, ninajivunia kuwa na cheti cha Teknolojia ya Habari (ICT), kutoka taasisi pekee inayotoa kozi hii katika kijiji kizima, na nimeajiriwa kwa furaha," anaongeza.
Wakati wa mafunzo ya ujuzi wa miezi 3-6 katika Vituo vya jamii, wakimbizi na Watanzania kutoka vijiji vya karibu hujifunza bega kwa bega, kuingiliana kwa uhuru, na kujifunza kutoka kwa kila mmoja. “Nilikutana na watu wapya na kupata marafiki wapya miongoni mwao, wakimbizi. Ni watu kama wewe na mimi; kinachotutofautisha sisi (Watanzania) na wao (wakimbizi) wanaishi kambini wakati sisi tupo nyumbani ambako tunaweza kufanya mazoezi baada ya masomo,” alisema Sporah.
"Upatikanaji wa riziki hupunguza utegemezi wa wakimbizi kwenye misaada ya kibinadamu na huongeza kujitegemea miongoni mwa jamii," Peter Opio, Afisa wa Kimaisha wa UNHCR alisema. "Kupanua huduma kwa jumuiya inayowapokea huchangia katika kukuza kuishi pamoja kwa amani na huongeza mshikamano wa kijamii kati ya wakimbizi na jumuiya zinazowahifadhi wakimbizi kulingana na matarajio ya Mkataba wa Kimataifa wa Wakimbizi," aliongeza.
Kiongozi wa Kijiji cha Nengo Bw.Jumanne Rashid aliongeza kuwa kituo hicho cha mafunzo kimefungua milango kwa vijana wengi katika eneo lake na kuwasaidia kujitegemea jambo ambalo ni muhimu katika kupunguza umaskini katika ngazi ya wilaya. Kiongozi huyo wa kijiji alitoa wito kwa UNHCR na washirika kuendelea na msaada huo kwani unawasaidia kufikia malengo yao ya maendeleo.
Vituo vya Jamii vilivyoundwa mwaka 2017 chini ya Mpango wa Pamoja wa Umoja wa Mataifa Kigoma (KJP), kwa ufadhili wa Serikali ya Norway, vimechangia chanya katika maisha ya watu 3,764 (wanawake 2,017). Zaidi ya asilimia 15 (570) ya wahitimu walikuwa raia wa Tanzania kutoka vijiji vya jirani. Kupitia KJP, UNHCR, na watendaji wengine wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakifanya kazi ili kufikia matokeo ya pamoja ambayo yanapunguza mahitaji, hatari, na udhaifu wa jamii katika mkoa wa Kigoma uliokusanywa kwa miaka mingi.