Wazee wanufaika na mradi wa kuhudumia magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) -Nyarugusu
Uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii katika kujua dalili na kupata vipimo kwa wakati inaweza kusaidia kuokoa Maisha ya mtu mwenye magonjwa yasiyoambukiza has
Wazee wanufaika na mradi wa kuhudumia magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) -Nyarugusu
Na Maimuna Mtengela
Uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii katika kujua dalili na kupata vipimo kwa wakati inaweza kusaidia kuokoa Maisha ya mtu mwenye magonjwa yasiyoambukiza hasa kisukari.
“Afya yangu imeimarika zaidi baada ya kuanza kupata matibabu na chakula cha ziada baada ya kugundulika kuwa nasumbuliwa na Ugonjwa wa kisukari” anasema Elongo Byosaa.
Elongo Byosaa (71) na mume wake Ramazani Yangya (75), ni wakimbizi wanaoishi katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Katika nyakati tofauti, familia hii iligundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari mwezi wa kwanza mwaka 2022. Shukrani kwa mradi wa World Diabetes Foundation (WDF) unaolenga kuasaidia wagonjwa wa kisukari kambini kwa kipindi cha miaka mitatu.
Mwanzoni mwa mwaka 2022 kwa vipindi tofauti familia hii imekua ikipata maumivu makali ya kichwa, uchovu, kwenda haja ndogo mara kwa mara, kiu na mabadiliko ya uzito yaliyosababisha kushindwa kumudu shughuli zao za kila siku hali ambazo zinatambuliwa kama dalili za Ugonjwa wa kisukari. Hata hivyo, Ramazani amepata upofu wa macho ambao umepelekea familia yao kuwa tegemezi.
Elongo na mume wake walikimbia kutoka Kongo miaka ya 1990 kutokana na machafuko yaliyotishia usalama wa maisha yao na Jamii kwa ujumla. Elongo anakumbuka kusikia “milio ya risasi, kelele za mapanga, vilio na kuona miili ya watu waliopoteza maisha ikiwa imetapakaa damu” Watoto wao watatu waliuwawa kikatili. Elongo na mume wake walifanikiwa kukimbia wakiwa na wajukuu wawili na vitu vichache ikiwemo picha moja ya familia.
Kila mwaka, tarehe 14 Novemba, dunia huadhimisha Siku ya Kisukari duniani ili kujenga uelewa kwa jamii juu ya ugonjwa huu. Takwimu kutoka shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa, takribani watu milioni 422 duniani wanaugua kisukari, wengi wao wakiwa ni kutoka nchi zenye uchumi wa chini na uchumi wa kati. Kwa wastani vifo milioni 1.5 vinavyohusishwa na kisukari hutokea kila mwaka. Hata hivyo, idadi ya wagonjwa wa kisukari pamoja na vifo huongezeka kila mwaka.
Zaidi ya wakimbizi 6,138 katika kambi ya Nyarugusu, na wazawa 760 wameweza kuonana na wataalamu na kupata ushauri wa afya. Elongo na mume wake walianza matibabu mara tu baada ya kufanya vipimo mapema mwaka huu.
Kama sehemu ya kukabiliana na magonjwa sugu, Shirika la Kimataifa Linalohudumia Wakimbizi - UNHCR Pamoja na wadau wengine kupitia mradi wa WDF wanatekeleza Shughuli mbalimbali zinazolenga kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutambua mapema dalili za magonjwa yasiyoambukiza hususani kisukari. Pia wanatoa mafunzo kwa wahudumu wa afya, pamoja na chakula cha ziada kwa wale wanaobainika kusumbuliwa na maradhi hayo. Aidha uwepo wa huduma za kuonana na wataalamu wa afya ndani ya kambi ni jambo ambalo limewapatia wakimbizi na wazawa nafuu.
Akiongelea juu ya mabadiliko yao, Ramazani anasema “Ninapokea mlo wa ziada kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya. Huwa napokea matunda na mboga mboga kama chakula cha ziada mbali na unga, maharage, mafuta ya kupikia na vingine vinavyotolewa na Shirika la Chakula Duniani (WFP)”. Ramazani anaamini chakula cha ziada kimesaidia kuimarisha afya yake na kupunguza athari za kisukari kwake na kwa wengine wenye tatizo kama lake kambini.
“Kisukari na magonjwa mengine yasiyoambukiza yanaendelea kuongezeka duniani na hivyo kuongeza shinikizo katika mfumo wa afya hasa kwa nchi zinazoendelea” Anaeleza Gideon Ndawula, Afisa afya UNHCR. Hili ni jukumu kubwa kwa mashirika yanayotoa misaada ya kibinadamu ambapo lengo kuu la awali ni kutoa huduma kwa magonjwa yanayoambukiza na magonjwa ya mlipuko.
Huduma za afya ikijumuisha magojwa yasiyoambukiza hutolewa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) katika hospitali kuu ya Nyarugusu na kituo cha cha afya. “huduma hii katika kituo kidogo cha afya inafurahiwa zaidi na jamii kwa sababu imesaidia kusogeza huduma karibu na maeneo wanayoishi” Anasema Dkt. Mohamed Abbas, Mratibu wa Afya TRCS.
“Ili kupunguza athari za magonjwa sugu na yasiyoambukiza ni vyema kuhakikisha kwamba Jamii inashirikishwa taarifa sahihi za kutambua dalili za awali lakini pia inahamasishwa juu ya umuhimu wa kufanya vipimo kwa wakati ili kupunguza athari za magonjwa hayo na hivyo kurahisihsa mfumo wa upatikanaji na utoaji wa huduma za afya” Anaongeza Gideon. Malengo ya mradi ni kuwafikia wakimbizi na waomba hifadhi 240,000 katika kambi za Nduta na Nyarugusu na wazawa 53,000.
UNHCR pamoja na wadau wake inatoa shukrani za pekee kwa WDF kwa kuwawezesha kutoa huduma za afya na elimu juu ya magonjwa yasiyoambukiza kwa wakimbizi na wananchi wa mkoa wa Kigoma. Msaada zaidi unahitajika ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi na kuweza kumudu changamoto mbalimbali ambazo bado zimekua kikwazo ikiwemo nguvu kazi na vifaa vya kuwawezesha wagonjwa kujipima wenyewe na kuweza kufuatilia maendeleo ya afya zao, rufaa na uboreshaji wa miundombinu ya afya.