Taarifa kwa vyombo vya habari

Grandi apongeza urejeaji wa wakimbizi wa Burundi, na kuhimiza misaada zaidi

10 Februari 2023

© UNHCR Tanzania Chanzo cha Picha

Bujumbura (Burundi) and Dodoma (Tanzania) - Wakati hali ya Burundi inaendelea kuimarika, Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi, Filippo Grandi, amesisitiza dhamira ya UNHCR ya kusaidia wakimbizi kurejea salama kutoka katika nchi walizopewa hifadhi.

Tangu mwaka 2017, zaidi ya wakimbizi 200,000 wa Burundi wamesaidiwa na UNHCR kurejea nchini kwao kwa hiari kutoka nchi jirani ikiwemo Tanzania.

Akihitimisha ziara yake ya siku mbili nchini Burundi, Grandi amemshukuru Rais Evariste Ndayishimiye kwa juhudi za kuleta utulivu nchini Burundi. 

“Tunaishi katika ulimwengu wenye fursa chache tu za kuweza kusaidia kutafuta suluhisho la kudumu kwa wale wanaolazimika kuyakimbia makazi yao. Mara nyingi, migogoro hudumu kwa muda mrefu lakini ninafarijika kuona wakimbizi wa Burundi wanafanya uamuzi wa kurejea nyumbani baada ya miaka mingi uhamishoni. Sote tunapaswa kufanya kazi ili kuhakikisha wanapata suluhisho la kudumu,” alisema Grandi. "Juhudi za Serikali ya Burundi na wadau katika kusaidia wakimbizi wa Burundi wanaorejea nyumbani zinatia moyo sana."

Grandi ametembelea eneo la Rugombo na kuonana na baadhi ya wakimbizi ambao wamerejea nyumbani hivi karibuni na kushuhudia misaada inayotolewa na UNHCR na wadau ili kuwawezesha kujenga upya maisha yao.  Misaada inajumuisha usafiri, chakula, fedha taslimu, na vifaa vya nyumbani kwa wakimbizi wanaorejea Burundi. Kwa kuzingatia ukubwa wa mahitaji, UNHCR imeamua kuboresha na kuimarisha misaada kwa wanaorejea.

“Hata hivyo, tunahitaji wadau wa maendeleo kusaidia  kuboresha upatikanaji wa huduma, na shughuli za kijamii kwa wakimbizi wanaorejea. Hawa ni raia wa Burundi na wanahitaji kujumuishwa katika mipango ya maendeleo” Grandi aliongeza.

Burundi pia inahifadhi wakimbizi 80,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Grandi ametembelea kituo cha wakimbizi cha Cishemere kilichopo Kaskazini Magharibi mwa nchi na katika eneo linalopakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kukutana na wakimbizi wanaokimbia machafuko na ukatili Mashariki mwa DRC.

Grandi amewasili mkoani Dodoma leo akitokea Burundi na kufanya mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa, ni hatua za mafanikio zinazoendelea kutekelezwa katika kuboresha mazingira na mahitaji nchini Burundi kwa wale wanaoendelea kurejea.  Grandi pia ameshukuru utamaduni wa muda mrefu wa Tanzania wa kukaribisha wakimbizi na juhudi zinazoendelea za kuwahudumia wale wanaokimbia migogoro na mateso.

Kwa takwimu, Tanzania inahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi wa Burundi duniani. Takribani wakimbizi na waomba hifadhi 248,000 wengi wao kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaishi Tanzania.

 "Shirika litaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali, Mashirika, na wafadhili, pamoja na wadau wa maendeleo, ili kuhifadhi na kutafuta suluhisho kwa wale wanaolazimika kuyakimbia makazi yao.” alisema Grandi.

Katika muktadha huo, UNHCR inapokea kwa furaha tangazo la Umoja wa Ulaya la kutoa ufadhili wa Euro milioni 40 katika miaka ijayo kwa washirika wanaosaidia kuboresha mazingira ya urejeaji nchini Burundi. Ufadhili huo utawanufaisha wakimbizi wa Burundi katika ukanda huu, pamoja na wale waliorejea nyumbani, kwa kuhakikisha wanapata usaidizi wanaohitaji ili kuishi kwa usalama na heshima. Ufadhili huo utajumuisha ulinzi na uthabiti, msaada wa kisheria, masuala ya ukatili wa kijinsia, ujuzi wa kusoma na kuandika na shughuli za kilimo.

MWISHO.

 

Kwa mawasiliano Zaidi:

Chadi Oanes, ouanes@unhcr.org , +255 755 314 549

Goodness Mrema, mremag@unhcr.org +255 714 058 749

Goodness Mrema

Goodness Mrema

UNHCR
Afisa wa Mawasiliano

Mashirika ya UN yanayojihusisha katika Huu Mpango kazi

UNHCR
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa

Malengo yanayofanyiwa kazi kupitia mpango huu