Japan na UNHCR zatia saini makubaliano ya $360,000 ili kusaidia wakimbizi wanaowasili Tanzania kutoka Kongo
12 Februari 2024
Serikali ya Japan na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), leo zimetia saini makubaliano mapya ya ushirikiano utakaowezesha utoaji endelevu wa huduma muhimu ikiwemo malazi, maji safi na salama, na usafi wa mazingira, kwa wakimbizi wanaoendelea kuwasili mkoani Kigoma nchini Tanzania wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Mchango wa dola za Kimarekani 360,000 kutoka kwa Serikali na watu wa Japan utasaidia kuimarisha huduma za dharura za kuokoa maisha kwa watu wanaokimbia machafuko nchini DRC.
“Wakati Japan, na UNHCR, wanafanya jitihada za kuisaidia Tanzania, natumaini kwamba serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza jukumu la kutoa hifadhi na huduma muhimu kwa wakimbizi kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu. Kwa kufanya kazi pamoja, tunaweza kuleta matokeo chanya, na kuhakikisha mustakabali mzuri na salama kwa maisha ya wakimbizi,” alisema Bw. Yasushi Misawa, Balozi wa Japan nchini Tanzania.
Mwaka 2023, UNHCR na washirika wake wa kitaifa na kimataifa kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walipokea zaidi ya wakimbizi 14,400 mkoani Kigoma ambao walipewa huduma mbalimbali ikiwemo mahali salama pa kulala, chakula, maji na misaada mingine ya kibinadamu. Mara nyingi wakimbizi na watu wanaolazimika kukimbia makazi yao hufika sehemu salama wakiwa na vitu vichache tu walivyoweza kubeba mikononi mwao pamoja na nguo walizovaa tu. Uwepo wa makazi, maji safi na salama na vifaa vya usafi wa mazingira, kutasaidia kudumisha usafi kwenye maeneo wanayoishi wakimbizi na kupunguza maradhi na vifo.
“Mwaka jana, nilitembelea kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyopo mkoani Kigoma, na niliweza kuzungumza na wanaume, wanawake na watoto waliokimbia kutoka DRC. Ni watu kama mimi na wewe, waliokata tamaa, walikuwa wakilia kwa kupoteza wapendwa wao, kukosa marafiki, na majirani. Mchango wa Japan utatuwezesha kuwasaidia wakimbizi kuishi maisha yenye utu wakiwa uhamishoni,” alisema Bi. Mahoua Parums, Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania.
UNHCR inahitaji dola milioni 8 ili kuweza kukidhi mahitaji ya wakimbizi kutoka DRC, na inaendelea kuziomba jumuiya za kimataifa kuchangia misaada ya kibinadamu kadiri mahitaji yanavyozidi kuongezeka. Kufikia tarehe 31 Desemba 2023, Tanzania inahifadhi zaidi ya wakimbizi 240,000, wengi wao kutoka Burundi na DRC. UNHCR inawashukuru sana watu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wamekuwa mfano wa kimataifa katika kupokea na kuhifadhi wakimbizi. Ni muhimu kuendelea kudumisha mshikamano kati ya wakimbizi na jamii zinazowapokea.
Mwisho.