Zaidi ya matone mawili: Watu na juhudi nyuma ya kampeni ya chanjo ya polio
Na Sarah Mujulizi
Kwa mama anayemshuhudia mtoto wake akipewa matone mawili ya chanjo ya polio, tukio hilo huchukua sekunde chache tu. Lakini nyuma ya matone hayo mawili kuna juhudi kubwa zaidi: mamlaka za afya zinazopanga kampeni, viongozi wa jamii wanaohamasisha familia, wahudumu wa afya wa jamii wanaotembea kaya kwa kaya , watoa chanjo wanaotoa chanjo, timu za takwimu zinazofuatilia maendeleo, na wasimamizi wanaochukua hatua pale mapungufu yanapoonekana.
Wakati wa kampeni ya chanjo ya polio nchini Tanzania, watu hawa huunda mnyororo wa juhudi unaoanza muda mrefu kabla mtoa chanjo hajafika kwenye kaya.
Inaanza na mipango na uongozi
Muda mrefu kabla timu za chanjo hazijaingia kwenye jamii, viongozi wa Serikali, wakiwemo mamlaka za afya za kitaifa, kikanda na wilaya, wakishirikiana kwa karibu na washirika kama Gavi, Muungano wa Chanjo, UNICEF na WHO, hupanga timu, vifaa, uhamasishaji wa jamii na ufuatiliaji ili kuhakikisha watoto wanafikiwa, wakiwemo wale walio katika maeneo magumu kufikika.
Kwa Dkt. Andrew Method, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, kampeni yenye mafanikio huanza na maandalizi.
“Tunapohakikisha kwamba wananchi wa Manyara wanapata huduma bora za afya, tuna kampeni inayolenga kuwalinda watoto dhidi ya polio. Ili tufanikishe hili, kampeni ya chanjo yenye mafanikio lazima ianze na maandalizi. Tunahitaji kujua watoto wako wapi, timu zetu zinapaswa kwenda wapi na wanahitaji msaada gani ili kufikia kila jamii, ikiwemo maeneo ambayo ni magumu kufikika.”
Lakini mipango pekee haitoshi. Mafanikio ya kampeni pia yanategemea imani na ushiriki wa jamii.
Kabla mtoa chanjo hajabisha hodi
Viongozi wa jamii na viongozi wa dini husaidia kuunganisha kampeni na familia, kwa kutoa taarifa, kuhamasisha wazazi na walezi kushiriki, na kujibu maswali au wasiwasi wao.
Mchungaji Amos Z. Nahhato, Kanisa la Elim Pentecostal, Babati, anasema sauti zinazoaminika katika jamii zinaweza kusaidia familia kuelewa kile wanachoweza kutarajia.
“Watu husikiliza taarifa inapowafikia kupitia mtu wanayemfahamu na kumwamini. Tunasaidia kueleza lini timu za chanjo zitafika na kwa nini ni muhimu wazazi kuwaandaa watoto wao wawepo.”
Jamii ikiwa imepata taarifa, kazi huhamia mlangoni mwa kaya.
Kutoka nyumba hadi nyumba
Kwa wahudumu wa afya ya jamii, kuwafikia watoto kunamaanisha kwenda zaidi ya vituo vya afya na kufika kwenye maeneo wanayoishi familia.
Agnes Frednand Njaiko hutoka nyumba moja hadi nyingine, akiwatambua watoto wanaostahili chanjo, akizungumza na walezi na kusaidia kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa.
“Kazi yetu si kubisha tu hodi. Tunapaswa kumweleza mlezi kwa nini chanjo ni muhimu, kujibu maswali yake na kuhakikisha tunampata kila mtoto anayestahili chanjo.”
Wakati mwingine hilo humaanisha kurudi kwenye kaya endapo mtoto hayupo.
“Wakati mwingine unafika na mtoto hayupo, hivyo unapaswa kurudi tena. Huwezi kusema tu hatukumkuta mtoto na kuendelea na kaya nyingine.”
Mtoa chanjo anapofika
Kwenye kaya, kampeni huonekana moja kwa moja. Mtoa chanjo humtambua mtoto, hutoa chanjo na kurekodi taarifa za chanjo kabla ya kuelekea kwenye kaya inayofuata.
Kwa Ester Njidile, kutoa matone mawili ni sehemu moja tu ya jukumu.
“Kutoa matone mawili huchukua sekunde chache tu, lakini tunapaswa kuhakikisha tumempata mtoto sahihi, tumempa chanjo kwa usahihi na tumerekodi taarifa kabla ya kwenda kwenye kaya inayofuata.”
Kisha timu inaendelea na safari.
Kubadilisha taarifa kuwa hatua
Wakati watoa chanjo wakipita katika jamii, timu ya usimamizi wa takwimu hufanya kazi nyuma ya pazia. Taarifa zinazokusanywa katika maeneo ya utekelezaji husaidia kuonyesha timu zimefanya kazi wapi, watoto wangapi wamefikiwa na maeneo ambayo huenda bado yana mapungufu.
Timu ya takwimu hukagua na kukusanya taarifa hizo ili timu za programu ziweze kufuatilia maendeleo na kuchukua hatua pale mapungufu yanapojitokeza.
Elizabeth Changendo, Meneja wa Takwimu, anaeleza:
“Taarifa zinazotoka kwenye maeneo ya utekelezaji zinatuonyesha kinachoendelea kwenye jamii. Jukumu letu ni kuhakikisha taarifa hizo ni kamili, sahihi na zinapatikana kwa wakati ili timu ziweze kuchukua hatua.”
Taarifa hizo huwasilishwa tena kwa wasimamizi walioko kwenye maeneo ya utekelezaji.
Erick Bunziya Peter, msimamizi wa timu, hutumia taarifa hizo pamoja na alichokiona uwanjani kubaini maeneo ambayo timu zinaweza kuhitaji kufuatilia zaidi.
“Jukumu langu ni kujua timu ziko wapi, zinakutana na nini na kama kuna watoto ambao bado hawajafikiwa. Ikiwa kuna tatizo, tunahitaji kulishughulikia wakati kampeni bado inaendelea.”
Taarifa zinapoonyesha kuwepo kwa mapungufu, timu zinaweza kuchunguza, kurudi kwenye kaya na kuendelea kuwatafuta watoto ambao huenda hawakufikiwa.
Ni mzunguko endelevu: kufikia, kurekodi, kupitia na kuchukua hatua.
Kiini cha yote: familia
Kwa walezi, kampeni ni rahisi zaidi: mhudumu wa afya anafika nyumbani, anaeleza sababu ya ziara na kuwaomba wampatikane mtoto kwa ajili ya chanjo.
Jamila Eddy alipokea timu ya chanjo nyumbani kwake Magugu, Babati.
“Walipofika, nilisikiliza maelezo yao. Nilitaka kuelewa kwa nini mtoto wangu alihitaji chanjo. Nilikuwa na maswali mengi, na mtoa chanjo alinielezea. Hilo lilinipa ujasiri wa kumruhusu mtoto wangu apewe matone.”
Uzoefu wake unairejesha kampeni kwenye jambo muhimu zaidi: mtoto.
Kutoka kwenye mipango ya kikanda na uhamasishaji wa jamii hadi ziara za nyumba kwa nyumba, utoaji wa chanjo, ukusanyaji wa takwimu na ufuatiliaji, kila sehemu ya mnyororo huu inachangia kuwafikia watoto.
Zaidi ya matone mawili
Kwa familia, ziara ya chanjo inaweza kuchukua dakika chache tu. Lakini kwa watu walio nyuma yake, kufika kwenye mlango huo ni matokeo ya mipango, uhamasishaji, safari, mawasiliano, utoaji wa chanjo, ukusanyaji wa takwimu, usimamizi na ufuatiliaji.
Kisha timu inaendelea na safari, kwenda kwenye kaya inayofuata, na kumfikia mtoto anayefuata.
Kwa sababu nyuma ya kila matone mawili kuna juhudi kubwa zaidi: jamii na mfumo wa afya wakishirikiana kuwafikia watoto na kuimarisha ulinzi dhidi ya polio.
“Kampeni yenye mafanikio ya chanjo inategemea uongozi imara wa Serikali na juhudi za pamoja za wahudumu wa afya, jamii na washirika. WHO inaendelea kutoa msaada wa kitaalamu katika kuimarisha mifumo inayosaidia Tanzania kuwafikia watoto kwa chanjo ya polio na kutumia taarifa za kampeni kubaini na kushughulikia mapungufu,” alisema Dkt. Alex Gasasira, Mwakilishi wa WHO nchini Tanzania.