Kilimo Cha Hali Ya Hewa: Uwekezaji Katika Uzalishaji Wa Mtama Huboresha Usalama Wa Chakula Na Mapato Kwa Wakulima Wadogo
.
Katika mkoa wa Dodoma wenye hali ya ukame katikati mwa Tanzania, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linashirikiana na wakulima wadogo wadogo ili kuboresha uwezzo wao wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji wa masoko. Hii imekuwa na athari ya kichocheo kwenye soko la mtama huku mtama wenye ubora wa juu unaotafutwa na viwanda vya bia vinavyowapa wakulima uhakika wa soko kwa bei ya juu. WFP pia inanunua mtama moja kwa moja kutoka kwa wakulima hawa kwa ajili ya operesheni zake nchini Sudan Kusini.
Chini ya ufadhili wa Msaada wa Ireland, WFP ilianzisha Mradi wa Kilimo cha Hali ya Hewa (CSAP) katika vijiji 218 katika wilaya sita za Dodoma, yaani, Bahi, Chamwino, Chemba, Kondoa, Kongwa na Mpwapwa. CSAP inawawezesha wakulima wadogo wadogo kufanya uzalishaji endelevu na elimu ya soko kupitia mafunzo katika utendaji mzuri wa kilimo pamoja na usimamizi na uhifadhi wa baada ya mavuno.
Wafanyabiashara wanaotafuta masoko ya kikanda wananufaika na mavuno bora na mazao bora, huku mapato yakiingia moja kwa moja mifukoni mwa wakulima wadogo. Mwaka 2021 pekee, WFP ilinunua mtama wenye thamani ya dola milioni 4.4 kutoka kwa wakulima wanaosaidiwa na CSAP. Lengo la awali la mpango huo lilikuwa kuongeza mazao yanayoweza kufanya biashara hadi tani 10,000 (mt) ifikapo mwaka 2022 na ilikuwa imefikia zaidi ya 25,000 mt mpaka mwaka 2021.
Kijiji cha Kisima ni mfano mzuri wa manufaa ya CSAP. Kijiji hicho kilichopo katika Wilaya ya Mpwapwa, kina idadi ya watu zaidi ya 4,000 kati yao zaidi ya 1,600 ni wakulima wenye uwiano wa wanaume na wanawake 50:50. Ndani ya miaka miwili tangu kuanza kwa mradi, kumekuwa na ongezeko la uzalishaji kwa kuwa wakulima walizingatia taratibu mpya za kilimo ikiwa ni pamoja na matumizi ya mbegu bora zilizothibitishwa, mbolea, mzunguko wa mazao na matumizi ya mashine za kupukuchua ili kupunguza upotezaji wa baada ya mavuno. Katika msimu wa 2019, mavuno ya mtama katika kijiji cha Kisima yalikuwa kilo 600 kwa kila ekari. Mwaka 2021, uzalishaji uliongezeka hadi wastani wa kilo 800-900 kwa ekari na kuongeza mapato ya wakulima. Wakulima wana usalama wa chakula, na kaya zimekuwa na nguvu zaidi. Mradi huo umebadilisha maisha yao kwa njia nyingi.
Kuwaunganisha wakulima moja kwa moja na wanunuzi kumeondoa soko kwa watu wa kati na kuongeza sehemu ya mapato yanayokwenda kwa kaya za kilimo. Bei ya sasa ya mtama – Tsh. 550 kwa kilo - ni ya juu zaidi kwa wakulima katika kijiji hicho kuwahi kupata kutoka kwa wanunuzi binafsi. Hii ni ongezeko la asilimia 120 ikilinganishwa na viwango vya soko vilivyokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa CSAP. "Hii haijawahi kutokea katika maisha yangu hapa kijijini," alisema mwenyekiti wa kijiji cha Kisima.
Kijiji cha Kisima kimepata matokeo ya ziada kutokana na faida hizi kama vile kuongezeka kwa shughuli za kuzalisha kipato kupitia bustani ya mboga na ufugaji mdogo wa wanyama. Zaidi ya hayo, wakazi zaidi wanajenga nyumba za kisasa wakati wakulima zaidi wanabadilika kutoka kwenye nyumba zilizoezekwa kwa nyasi hadi nyumba za mabati.