Vinara wa mabadiliko wanaopambana na ukatili wa kijinsia nchini Tanzania
.
Rahabu alikuwa na umri wa miaka 17 pale alipopata mimba na kuacha shule, jambo lililokatisha ndoto yake ya kuja kuwa mwalimu. Alirejea kwao katika maji wa Kahama akiwa na miaka 22, baada ya kuachana na mumewe aliyekuwa akimtesa – na sasa akiambatana na watoto wawili – na alishiriki na kuhitimu katika Mradi wa Wasichana wa Umri wa Balehe – ambayo ni programu iliyoanzishwa na Kiota Women's Health and Education (KIWOHEDE) kwa msaada wa UNFPA. Mradi huo unalenga kuwasaidia wasichana waliokatisha masomo yao katika Mkoa wa Shinyanga, kwani mkoa huo ni miongoni mwa mikoa yenye viwango vya juu vya watoto wanaokatisha maomo yao nchini Tanzania.
Leo hii, Rahabu ana kipindi chake cha redio na ni mwanaharakati, akiwaelimisha wanarika wenzake kuhusu umuhimu wa wasichana kuendelea na masomo shuleni. Anatoa changamoto kwa mitazamo waliyo nayo vijana katika jamii yake huko Kahama, akiwasaidia kuhojji imani kwamba mwanamume ana haki ya kutenda ukatili au ikiwa msichana ananyanyaswa, basi alitenda kitu kilichomchokoza mtesi wake.
Rahabu alikuwa mmoja wa vinara 16 waliopata tuzo katika sherehe zilizofanyika mapema Desemba jijini Dar es Salaam katika tukio lililoandaliwa na mashirika ya Women in Law & Development in Africa (WiLDAF) na Coalition Against Gender-Based Violence (MKUKI) – kwa ufadhili wa UNFPA na Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania – kama sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati wa Kukomesha Ukatili dhidi ya Wanawake.
Vinara hao 16 wa mabadiliko, waliochaguliwa kupitia mchakato wa upendekezwaji, walitokea katika nyanja mbalimbali za maisha – na wana hamasa tofauti inayowasukuma kutaka kushiriki katika kukomesha ukatili kwa msingi wa kijinsia – lakini wana kitu kinachofanana: wote ni watu wa kawaida wanaofanya mambo ya kipekee, ambapo wanatumia vipawa vyao kukabiliana na ukatili wa kijinsia na wanongezea idadi ya vuguvugu lenye nguvu la kitaifa. Kuanzia kiongozi wa kiroho wa Zanzibar, kijana mwanaharakati wa Shinyanga hadi msanii wa hip hop wa jijini Dar es Salaam – ujumbe wa vinara hawa kwa pamoja ni mkubwa na wa wazi – kama tukishirikiana, tutafikia katika mabadiliko tunayotaka – dunia iliyo sawa zaidi kwa kila mwanamke na kila msichana kokote ulimwenguni.
Licha ya maendeleo yaliyopatikana nchini Tanzania, data zinaonyesha kwamba ukatili dhidi ya wanawake na watot bado uko katika viwango vya juu visivyovumilika; kukabiliana na tatizo kubwa kiasi hiki kunahitaji mwitikio mkubwa vilevile. Kama sehemu ya maadhimisho ya Siku 16, WiLDAF na MKUKI – kwa mara nyingine wakiwa wanafadhiliwa na UNFPA na Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania – pia waliandaa majadiliano ya kidini huko Zanzibar kwa ajili ya wazee wa kutoka imani zote – ambao hawa ni washirika muhimu katika kusukuma maendeleo ya haki za wanawake na wasichana nchini Tanzania. Viongozi wa kidini waliotoa ahadi ya pamoja iliyotiwa saidi ikiahidi kuongeza juhudi za kukomesha ukatili wa kijinsia na vitendo vyote vinavyoleta madhara katika jamii zao.
Tunapoingia mwaka 2021, ambapo tarehe ya ukomo wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu mwaka 2030 unazidi kukaribia, UNFPA inaendelea kuazimia kufikia katika ahadi yetu ya dunia na tutaendelea kusaidia juhudi za jamii; kwa kushirikiana, kutumia rasilimali, kufanya zaidi na zaidi na kufanya vizuri zaidi ili kufikia hatma tunayoitaka: dunia iliyo salama zaidi, bora zaidi kwa kila mwanamke na msichana.