Ikifadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Korea (KOICA) kama sehemu ya mradi wake wa kuimarisha ubora wa Elimu ya Shule za Sekondari (EQSSE) katika Zanzibar, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi (UNOPS) inashirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (MoEVT) huko Zanzibar kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa sayansi katika shule za sekondari. Mradi huu unasaidia Lengo la Maendeleo Endelevu la Umoja wa Mataifa (SDG) namba 4 kufikia elimu bora kwa wote ifikapo mwaka 2030 na unaendana na Dira ya Serikali ya Tanzania ya 2025.
UNOPS inaisaidia KOICA katika kutekeleza mradi wa EQSSE wa kuboresha maabara za sayansi ambapo miundombinu au vifaa havitoshi kwa ajili ya ubora katika kujifunza - hii imetambuliwa kama changamoto kubwa kwa Elimu ya Sekondari ya Zanzibar. Kwa ufadhili wa dola milioni 3, UNOPS imejipanga kujenga maabara za sayansi na vifaa vya kusambaza kwa shule kumi za sekondari Pemba, Unguja na Tumbatu. Kazi ya ujenzi ilianza Aprili 2022 na itakamilika mwishoni mwa mwaka.
Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini Tanzania, Bw. Kyucheol Eo, alisema Serikali ya Jamhuri ya Korea itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika sekta mbalimbali, hasa katika sekta ya elimu. Bw. Eo anatumaini kuwa mradi huo utaboresha ubora wa madarasa ya sayansi na kuchangia katika kufanikisha mfumo mzima wa elimu.
Meneja Miradi na Mkuu wa Ofisi ya UNOPS nchini Tanzania, John Fofanah, alitoa shukrani zake kwa ushirikiano mzuri na KOICA, Alisisitiza ahadi za kupeleka maabara mpya za sayansi na vifaa na vitendanishi kwa madarasa ya fizikia, kemia, na biolojia huku akihakikisha miongozo yote ya kiafya, kiusalama, kijamii na kimazingira inazingatiwa kufanyika wakati wa ujenzi.