Uzinduzi wa Programu ya Pamoja ya Data kwa ajili ya Mabadiliko ya Dijitali katika Kilimo
25 Oktoba 2024
Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa wamezindua mradi mpya wa kilimo cha kidijitali ili kuongeza tija vijijini, kuboresha upatikanaji wa soko, na kuwawezesha wanawake na vijana.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Mataifa imezindua rasmi Mpango wa Pamoja wa Takwimu kwa Mageuzi ya Kilimo Kidijitali (2024-27) unaolenga kutumia teknolojia kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo nchini Tanzania, kuongeza uzalishaji na ustahimilivu kwa jamii za vijijini, hususan wanawake na vijana.
Mpango huu wa dola za Marekani milioni 3, unaoungwa mkono na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Mfuko wa Pamoja wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) wa Umoja wa Mataifa, utatekeleza matumizi ya majukwaa ya kidijitali kutoa takwimu za kilimo kwa wakati sahihi, kusaidia wakulima wadogo kupata taarifa, kuboresha upatikanaji wa masoko na kuimarisha mifumo ya ufanyaji uamuzi.
Mpango huu wa pamoja chini ya Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, utaanza kutekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Kigoma, Ruvuma na Manyara, ukilenga jamii zinazohitaji msaada wa kilimo, kuunda masuluhisho endelevu ya kidijitali, kuboresha miundombinu ya kilimo, na kukuza ushirikiano katika sekta mbalimbali ili kuleta mageuzi ya kilimo.
Mashirika ya UNCDF (Shirika la Umoja wa Mataifa linaloongoza mpango huu), FAO, na IFAD yatafanya kazi kwa karibu na Wizara ya Kilimo, mashirika mengine muhimu ya Serikali na wadau wengine, ili kwa pamoja kuendeleza mafanikio ya programu na kufikia malengo yake.
Akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kutatua changamoto za kilimo kwa njia za ufumbuzi wa kibunifu, Mkuu wa Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Bi. Shabnam Mallick, alisema: “Programu hii ya pamoja ni udhihirisho wa nguvu ya ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja, kwa msaada mkubwa wa Umoja wa Ulaya na wachangiaji wengine wa Mfuko wa Pamoja wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), tunafanya kazi katika kuwezesha jamii na wafanya uamuzi kwa takwimu na teknolojia zinazohitajika ili kuchapuza maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo.”
Usuli:
Mpango wa Pamoja wa Takwimu kwa Mageuzi ya Kilimo Kidijitali unafadhiliwa na Mfuko wa Pamoja wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) wa Umoja wa Mataifa chini ya Mwelekeo wa Athari-Chanya za Kidijitali. Ni ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na mashirika ya Umoja wa Mataifa, lengo likiwa kuongeza kasi ya matumizi ya ubunifu wa kidijitali katika kutatua changamoto za kilimo, kuongeza uzalishaji na kukuza ukuaji wa uchumi jumuishi.
Mpango huu wa Pamoja umewezeshwa na michango ya ukarimu ya Mfuko wa Pamoja wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) kutoka Umoja wa Ulaya na Serikali za Ubelgiji, Denmark, Ujerumani, Ireland, Italia, Luxembourg, Monaco, Uholanzi, Norway, Poland, Ureno, Jamhuri ya Korea, Saudi Arabia, Uhispania, Uswidi na Uswizi. Msaada wao unasukuma harakati za mageuzi kuelekea kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo 2030.